KUSAKA HUBA (DIBAJI)

January 12, 2021 Off By Paskali Watua

5b780abd36def94d2cc0c6feab2201f3.jpg

Fasihi Brand Presents:
HADITHI: KUSAKA HUBA!
By
PASKALI NULL WATUA (MWANAFALSAFA)
(Tamanio La Moyo)
© 2020

DIBAJI

Chozi lilifuuza na kumtoka. Mashavu yake yalijaa michirizi ya machozi ya huzuni. Hakuamini kabisa. Hakuamini yalikuwa yamemtokea tena katika aushi yake. Ilikuwa huzuni kubwa kwake. Hakutaka kuamini chochote. Hata hivyo, hakuwa na budi kuamini. Lilikuwa limeshatokea tena mbele ya macho yake.

“Kwa nini afanye hivi? Kwa nini amuumize kwa kufanya vile?”

Ni yakini alimpenda sana. Alimpenda kwa moyo wake. Alijitolea sabili na kummwaia maji kama mche mchanga. Akammwaia mbolea yenye rutuba. Akachipuka kwa kasi ya ajabu. Akanawiri na kusimama kititi kama uyoga katika biwi la taka. Mpole, alimpa karibu kila kitu. Si, mapenzi, si pesa, si mali, si majumba, si biashara. Sisemi.

Haya yote hayakuweza kuuyeyusha uyabisi wa Mirriam. Japo alivipokea kwa bashasha, bado moyo wake haukuwa kwa Mpole. Hakumpenda kama alivyokuwa akifikiri Mpole. Hili lilibainika wazi pale Mirriam alipomwacha na kwenda kucheza mchezo wa mapenzi na janadume jingine. Mpole akaumia. Moyo wake ukanyauka. Nafsi yake ikapoteza fahamu. Mpole akakonda kwa mawazo.

Ni lini Mpole atapata binti mzuri wa kumuita mpenzi? Binti atakayempenda na kumdhamini? Binti atakayempenda yeye bila kujali lolote kumhusu? Binti atakayempenda na kumwonjesha utamu wa mapenzi utakaoyafuta yote mabaya aliyoyafunda moyoni kuhusiana na mapenzi? Ni lini Mpole atampata mwanamke kufu yake? Mwanamke atakayemuenzi na kumwonyesha ubora wa mwanamke katika maisha?

Mpole alimpenda Mirriam kwa moyo wake wote. Alimpenda kwa kuwa alifikiri Mirriam ndiye chaguo la moyo wake. Alimpenda kwa kuwa alifikiri Mirriam alimuenzi kama alivyokuwa akimuenzi yeye. Alifikiri labda ipo siku wataishi pamoja waitane mume na mke. Alifikiri Mirriam alimpenda tu kwa mapenzi ya dhati tofauti na mabinti wengine waliokuwa wamecheza ukaribu naye. Alikisia labda pengine Mirriam angempenda yeye tu na wala sio mali yake. Kwa nujumu mbi, Mirriam kama mabinti wengine, aliyeyuka na kumwachia banguzi katika moyo wake. Mirriam aliondoka wakati ambapo Mpole alimhitaji zaidi ya zaidi. Wiki chache zilizopita, Mpole alikuwa amemfunulia kilichokuwa ndani ya moyo wake. Siri aliyokuwa ameificha, aliiweka wazi. Akampa Mirriam moyo wake. Moyo ambao alihitaji usomwe kama kitabu na mwisho wa yote, ugilidiwe kwa mapenzi ya kweli. Hata hivyo, mambo yaligeuka. Mirriam baada ya kuonja utamu wa pesa na kuvuna njenje si njenje, aliamua kuponda wa fisi na kuondoka bila kutimiza ahadi za uongo/ukweli alizomuahidi Mpole.

Ni lini binti mzuri ataubisha mlango wa moyo wake? Au ni wakati ambapo atakuwa amerishai masharubu si haba mashavuni pake?

Hii sio mara yake ya kwanza ya yeye kuachwa katika upweke eti kisa mapenzi na mabinti ambao alidhani wanampenda kama alivyokuwa akiwapenda. Alikuwa katika mahusiano takribani saba ya kimapenzi huku akiwapenda mabinti wote kwa moyo wake wote. Aliishi kwa matumaini kuwa, walimpenda kwa udhati kama alivyokuwa akipenda. Hata hivyo, kumbe fikra zake zilimdanganya.

Je, yalikuwa ni majaaliwa yake kuachwa vivyo hata akiwa na utajiri wake huo? Kwani mapenzi ni nini? Aliishi kujiuliza.

Hakika, Mpole alikuwa tajiri wa kupindukia. Pesa kwake hazikuwa tatizo. Ni juzi tu alikuwa amekisoma kitabu cha Maskini Maarufu. Kitabu ambacho kilikuwa kimempa utata wa kufikiri. Hakuelewa maana ya mada ile. Eti Maskini Maarufu? Aliposoma baadhi ya dibaji walizotoa wahariri, ndipo alipopambaukiwa kuwa, umaskini uliolengwa sio umaskini wa ukosefu wa pesa. Alipambaukiwa kuwa, utajiri haumaanishi mwisho wa umaskini au ufukara. Utata ulipomzidia, aliamua kukiacha tu. Aliacha chakula kikitokota chunguni, asijue chanzo cha mtokoto wake ni upi.

Read Also  Africa Haiku Prize 2020

Zaidi ya kuwa tajiri wa matajiri, alikuwa ni mtu maarufu sana nchini hata nje ya nchi. Wengi walitamani sana kuwa na maisha kama yake. Kwa kukisia tu, walifikiri kuwa maisha yake yalitawaliwa na raha za uki na maziwa. Kwani hawajui usemi wa wahenga? Usemi usemao kuwa nyumba nzuri sio mlango? Mpole yeye kwake maisha hayakuwa ya kuridhisha. Bado alikuwa maskini. Maskini maarufu. Umaarufu wa kuwa mtu tajika na tajiri ila maskini wa kukosa mapenzi ya dhati. Umaskini wa kuchezewa kayaya za chini kwa chini na mabinti. Umaskini wa kutojua ukweli na hila za wanawake anaowachumbia. Hili la mabinti kupenda kutompenda, lilimuumiza si haba. Moyo wake uliungulia kwa maumivu. Aliona labda aliumbwa ahangaike kwa ajili ya mapenzi. Hata hivyo, bado hakuridhika. Alikuwa na matumaini. Matumaini ya kumpata binti atakayempenda jinsi alivyo.

Kwa ghadhabu kuu, aliitwa fremu iliyohifadhi picha zake na Mirriam. Aliitazama picha ile kwa tabasamu pana kama ada yake; muongo na mlaghai mkubwa, kwa njuti zake, aliikanyaga fremu ile ya kioo. Alitoa sauti ya kukerwa. Kama hakuridhika, aliitwa rungu yake aliyoipenda na kuanza kuvibondabonda vioo vilivyokuwa vimetapakaa kwenye sakafu ya himaya yake.

“Arrgghhhhhh!” alitoa sauti huku akikimbia kwenye jokofu lililokuwa mkabala na alipokuwa amesimama. Alitwaa chupa ya pombe na kuanza kuibugia kwa hasira. Alipiga mafumba mazito mazito huku akilaani vitendo alivyowahi kutendewa na mabinti.

“Fuc’ ya Mirriam. Fuc’ ya all bitches and thy kind!” alilaani Mpole kwa hasira huku akiendelea kumeza mafumba makubwamakubwa ya pombe. Sio kupenda kwake kufanya haya la. Alitamani maisha ya kuishi kwa amani na utangamano mzuri na waja. Hata hivyo, kumbe dua yake haikumfikia Muumba. Aliona maisha yake aliumbwa tu kuteseka. Kuteseka kwa sababu ya mapenzi tu. Mapenzi ya bure. Mapenzi yasiyoweza kununuliwa. Kwa mara ya kwanza, aliona utajiri wake ni bure tu. Aliona kumbe pesa ni kitu dhaifu sana duniani. Kitu ambacho kamwe hakiwezi kununua kitu cha bure kama mapenzi.

Kwa sababu hii, aliruhusu tena milizamu yake kuchiriza machozi ya majonzi na simanzi. Kutopendwa na kuchezewa na mabinti tofauti kulimfika kooni. Afadhali maana kama yangemfika kichwani, habari za tanzia zingekuwa zimegonga vichwa vya habari. Aliamua tu kulia. Aliona kulia ndiko rafiki wake au hata mpenzi wake aliyeumbiwa na Mola. Mola asiye na kosa. Mola asiyeweza kulaumiwa madhali ajua sababu ya kila jambo kutokea.

Akiendelea na zoezi lake la kulia na kunywa pombe kwa kubugia, alisikia nyayo za mtu zikikaribia lango la himaya yake. Baada ya muda kiduchu, lango lilifunguka. Ukimya ulitawala kisha sauti ya kiumbe ikafuatia. Sauti ambayo ililandana sana na ya mpenzi wake Mirriam aliyeumbwa kwa mapenzi haramu. Mirriam ambaye alikuwa amemuahidi kuishi naye kwa tabu na dhiki. Mirriam ambaye alimuahidi kufa naye wakati wowote. Lakini mwisho wa yote, aliamua kumwacha pweke. Kumwacha pweke ateseka kwa sababu ya penzi. Kumbe kauli zake zilikuwa tu uongo uliofichwa ndani ya maneno yaliyoonekana ya kweli.

“Samahani mkubwa… Stakabadhi zimefika…”

“Toka nje!” Mpole aliropokwa kwa hasira bila kupepesa macho.

“Lakini na…!”

“Get the sh’t out of here bitch! I ain’t signing anything…!”

“Mkubwa, iwapo hutotia sahihi, tutapoteza mabilioni ya pesa. Kumbuka hii ni dili zaidi ya madili!”

“Mbona husikiii? Listen you bitch, from today hence forth, you are fired!” Mpole alizidi kuwaka. Baada ya kauli yake, kimya kilijiri. Sauti ya binti yule haikusikika tena. Kekevu tu ndizo zilizombainisha Mpole kuwa, sekritari wake alikuwa akilia. Hata hivyo, hakujua sababu yake kulia kati ya kufukuzwa kazini au kukosa kutia sahihi kwenye stakabadhi ambazo zingeletea kampuni mabilioni ya darhimu.

Read Also  7 Must Do Tasks When Your Manuscript Is Finished

Maskini mtoto wa watu. Haikuhalisi apigwe kalamu kwa maneno hayo machache, akizingatia urefu wa barua yake ya kuomba kazi. Afadhali hata angepigwa kalamu kwa kupewa barua yenye maandishi hata mistari mitatu au minne. Lakini kwa wakati huo, hakuwa na budi kuondoka. Taratibu, aliurejesha mlango na kutokomea. Huo ukawa mwisho wake kwenye kazi katika kampuni hiyo ya Lion Empire Precious Agency Limited.

Hasira wanasema ni hasara. Maamuzi ya haraka huchukuliwa kama udhaifu. Hata yeye, Mpole, hakuamini kabisa kama alikuwa amempiga kalamu sekritari wake ambaye alikuwa amefanya kazi katika ofisi yake kwa miaka saba. Kando na dada yake ambaye alikuwa akiishi Marekani jijini New York, sekritari yuyu huyu ndiye alichukua nafasi ya dada yake. Alikuwa akicheza nafasi ya dada yake. Sio kwamba walikuwa wakichumbiana la. Walikuwa tu kama ulimi na meno. Hata pale ambapo Mpole alikuwa akiumizwa na mabinti wengine, sekritari huyu aliyejulikana kwa jina Rose, hakuacha kumliwaza na kumpa maneno ya matumaini. Hata Mpole alijua kuwa Rose ni mtu wa kipekee. Binti mrembo aliyeumbwa kwa bidii za mchwa. Madhali Rose naye alikuwa mwanamke, Mpole hakujirudi zaidi na kuona kafanya kosa. La! Alikuwa kakata kauli moyoni mwake. Kauli ya kuwachukia wanawake wote duniani isipokuwa mama yake na dada yake Susan Khai.

Akiwa pale ametulia, mlango ulifunguka. Mbele yake, alisimama wima mama yake. Uso wake ulikuwa umesawijika. Ni bayana alihisi maumivu yaliyokuwa yamemkumba mwanaye. Hivyo ndivyo mama wote walivyo. Nakisia tu. Si wanasema kuwa uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi?

Alisogea pembeni. Akachutama karibu na mwanaye ambaye alikuwa sakafuni huku akizungukwa na vigae vya chupa zilizovunjika. Machozi yalianza kumtoka. Simanzi si simanzi, ilimkumba ghafla baada ya kumwona mwanaye kakonda si haba.

Aliunyanyua mkonowe. Akaanza kumpapasa mwanaye mgongoni na hatimaye kumwinua. Mpole akaegemea kwenye bega la mama yake.

“Nimezipata habari. Mirriam anaolewa sio?” alianza mama mtu.

“Mam…”

“Shhhhhhhhhhh!” mama mtu alimkatiza.

“Usiseme lolote. Utajiumiza tu bure kwa wivu wa mapenzi,” mama aliongeza.

“Naona niliumbwa tu kuteseka kwa minajili ya mapenzi. Ni tajiri ndio ila, nimeona pesa haziwezi kununua mapenzi. Umaarufu sikwambii!”

“Mwanangu, mapenzi yapo. Najua utampata umpendaye kwa wakati mwafaka. Usiwe na shaka. Hujamsoma Paskali na kitabu chake Mwisho Wa Mwanzo?”

“Nimemsoma ila hayo nayaona tu mambo ya kubuni. Hayapo kwenye uhalisia huu tena duniani hapa penye madhila. Sasa? Naona mpenzi wangu wa dhati nitampata nikiwa wa umri wa miaka mia mbili tu. Wakati ambapo nakaribia kuifuata njia ya marahaba! Hata huyo nitakayempata wakati nimezeeka sitamaniki, hatokuwa na mapenzi ya dhati kwangu bali kwa mali yangu. Nitakapokufa na kufariki, basi itakuwa furaha kwake maadamu ana kila kitu ambacho hakukimwagia jasho!”

“Usiwe hivyo mwanangu. Usiwe na fikra hizo. Haya, Rose kanambia. Umempiga kalamu bila ya sababu. Usiruhusu hasira na maumivu yako kukuongoza kufanya maamuzi. Ni hatari sana,” mama alitulia na kuongeza, “unapaswa kutulia. Tuliza moyo wako ili tujue la kufanya mwanangu. Sitaki kukuona kwenye hali hii!”

“Kutulia? Mama unasema kutulia? Ah, mama. Nimesalitiwa si chini ya mara saba. Baya zaidi yule ambaye nilifikiri ndiye chaguo langu la moyo, ndiye yuyu huyu kaniachia donda kwenye moyo wangu!”

Read Also  Five Opportunities for African writers and poets for April 2020.

“Mwanangu, naelewa ila jua kuwa kuna mamilioni ya wanawake duniani ambao hata wapo tayari kwenda kwa waganga ili kukupata. Wengine wapo tayari hata kujitoa kafara kwa azma ya kukupata wewe tu!”

“Kunipata mimi au kupata pesa zangu?” aliuliza kibalagha na kutabasamu kwa bezo kubwa.

“Tunapaswa kufikiria jambo lingine. Nina wazo fulani!”

“Wazo lipi?” aliuliza Mpole huku akipiga fumba jingine la kinywaji chake.

“Kwanza, unapaswa kuiweka hii chini ili usikize kwa umakini!” mama alisema huku akimpokonya chupa ya mvinyo aliyokuwa akiing’ang’ania kukutu!

“Naona ni vyema ukaenda mbali na nchi hii. Uondoke hapa ili uweze kumsahau huyu Mirriam swila wa moyo wako!”

“Kuondoka?”

“Naam. Uondoke hapa. Azma yangu kuu, ni wewe kumpata mpenzi wa kweli na pili, ni hiyo sababu niliyokupa. Kumsahau Mirriam!”

“Mbona sikuelewi mama?”

“Huwezi kunielewa kwa sasa. Ninachotaka, uhame huku. Hata ikiwezekana uende nje ya nchi hii. Kutembea kwingi, ndiko kuona mengi. Katika hiyo tembeatembea, unaweza ukakumbana na mwanamke wa majaaliwa yako atakayekupenda na kukuthamini kwa hali zote.”

“Mama, naona kila mwanamke atakuwa wa majaaliwa yangu iwapo watamaizi kuwa mimi ni mkurugenzi mkuu wa kampuni ya “Lion Empire Precious Agency Limited.”

“Sio rahisi iwapo utavalia mwonekano tofauti na ulivyo sasa. Si wajua siku hizi wanawake wamekengeuka. Mavazi ya kupendeza, magari na pesa ndicho kichocheo kikubwa cha wao kujigandamiza kwa mtu kwa njia ya mapenzi. Nataka uwe tofauti. Uwe mtu wa hadhi ya chini tu kama mtu anayechuuza karanga mtaani. Uvalie mararuraru yaliyofumwa viraka si haba.” mama alitamka kauli ambayo ilimzindua Mpole katika bahari aliyokuwa kwayo.

“Ana maana gani huyu?” alijiuliza.

“Mama, sikuelewi kwa hakika.”

“Mwanangu, nataka uende nchi ya mbali. Mfano Marekani mji wa New York kule aliko dada yako. Huko, unaweza ukaanzisha kabiashara uchwara tu ka kuuza vitu vya hadhi ya chini kwa rejareja. Unaweza pia ukapanga chumba cha staha ya chini. Ukiwa hapo, naamini utampata mwanamke wa kufu yako maadamu wengi hawatotaka kujihusisha nawe madhali u mtu wa hadhi ya chini. Naomba uufiche uhalisia wako!”

Mpole alishangaa hadi ya kushangaa. Hakuamini kabisa kama mama yake angeweza kutoa kauli sampuli ile. Kauli ambayo kwake ilkuwa kauli isiyo na hadhi. Kauli ambayo kwake aliiona ya kujishusha kupitiliza kiasi.

“Mama, sidhani hilo ni suala muhimu na wazo lako, sioni kama litafanya kazi.”

“Kujaribu ndiko kuweza mwanangu. Usijali maana najua waogopa kujishusha. Iwapo utajinyenyekeza, basi naamini utajua ukweli kwamba, mapenzi ya kweli yapo. Unachohitaji ni utambulisho mpya wa kuuficha uhalisia wako. Baada ya hapo, utakuwa tayari kwa safari! Usijali kuhusu kubadili mwonekano wako. Najua pa kuwapata mafundi wa kubadilisha sura za watu. Tafakari kuhusu hilo,” mama mtu alisema na kunyanyuka. Alimpiga busu la kipajini na kutokomea. Alimwacha mwanawe kwa mawazo. Mawazo mazito ya kutafakari kauli zake nzito za kuanza harakati za kutafuta mapenzi. Mapenzi kwa mpenzi wa kweli atakaye mridhia na kuchukia kutomchukia Mpole kwa moyo wake wote!

“Kuzuru nchi tofauti kwa lengo la kutafuta mapenzi ya kweli?” aliwaza.

“Naona ni bora kujaribu kucheza na saikolojia za wanawake kama walivyokuwa wakinichezea.!”